Dar es Salaam. Mabingwa wa Tanzania, Yanga wamelazimisha sare 2-2 na URA ya Uganda katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mashabiki wa Yanga walisubiri hadi dakika ya 90, wakati mshambuliaji Jerryson Tegete alipofunga bao la kusawazisha baada ya mabeki wa URA kushindwa kuelewana na kipa wao.
Mshambuliaji wa URA , Lutimba Yayo aliifungia timu yake mabao mawili ya kuongoza katika dakika 42 na 51, kabla ya Didier Kavumbagu kuipatia Yanga bao katika dakika ya 66 na Tegete kuisawazishia Yanga.
URA walitawala vizuri kipindi cha kwanza ikiwa ni saa 24, tangu walipoichapa Simba kwa mabao 2-1 kwenye uwanja huo. Katika dakika ya 4, Derrick Walulya nusura aifungie timu yake bao baada ya shuti lake kupaa juu kidogo ya goli la Yanga.
Kipa mpya wa Yanga, Deogratias Munish ‘Dida’ alithibitisha ubora wake baada ya kuokoa shuti la Ngama Emmanuel akiwa ndani ya eneo la 18 katika dakika ya 27.
Yanga walimtoa Hamis Thabit na kumwingiza Bakari Masoud katika dakika 40, wakati URA waliwapumzisha, Joseph Owino, Ngama Emmanuel na kuwaingiza Munaaba Allan na Ike Obina.
Dakika tatu kabla ya mapumziko URA walipata bao la kuongoza lililofungwa na Yayo kwa shuti kali baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Yanga.
Waganda walirudi kipindi cha pili kwa nguvu zaidi na kufanikiwa kupata bao la pili lilililofungwa na Yayo kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya beki wa Yanga, Ibrahimu Job kumchezea vibaya Ngama Emmanuel katika dakika 51.
Mshambuliaji Kavumbagu alifungia Yanga bao la kwanza katika dakika 66, akiuganisha kwa kichwa krosi ya Juma Abdallah. Kocha wa Yanga, Ernest Brandts alimtoa Bahanuzi na kumwingiza Haruna Niyonzima katika dakika 77, ambapo mabadiliko hayo yalikuwa na faida kwa Yanga kwani iliwasaidia kurudi mchezoni.
CHANZO: MWANANCHI