Feature

Udaku wa Africa

Habari za Kimataifa

Habari za Kitaifa

Mapenzi

Michezo na Burudani

Udaku wa Ulaya

TIBAIJUKA AGOMA KUJIUZULU, ADAI YEYE HANA FASHION HIYO.


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka, akiongea na wanahabari hivi punde ndani ya Hyatt Regency Hotel Dar es Salaam amesema haoni sababu ya kujiuzulu kutokana na sakata la akaunti ya Escrow.
Aongeza kuwa watu wanaona suala la kujiuzulu kama fasheni ila yeye hayupo katika fasheni hiyo.

SAKATA LA ESCROW, KUMBE LUKUVI ALITAKA KUIBA RIPOTI SAA 9 USIKU.


Dar es Salaam. Viongozi wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na Deo Filikunjombe wamemtuhumu Waziri William Lukuvi kuwa alitaka kuiba ripoti ya kamati yao kuhusu uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Sakata hilo lilihitimishwa Jumamosi wakati Bunge lilipoazimia kuwajibishwa kwa watu wote waliohusika kwenye uchotwaji wa fedha hizo, ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa taasisi za fedha zilizoruhusu kufanyika kwa miamala mikubwa kinyume na taratibu za kibenki. Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao wawili kutoka Chadema na CCM walilieleza gazeti hili kuwa jaribio hilo lilishindikana baada ya wao na mjumbe mwalikwa, Luhanga Mpina (CCM) kuamua kukesha wakiilinda ripoti hiyo tangu ilipokuwa ikichapwa hadi ilipowasilishwa bungeni.
Hata hivyo, Lukuvi alikanusha vikali tuhuma hizo akisema kuwa aliipata ripoti hiyo siku iliposomwa na kwamba kama angehusika, asingekubaliwa kuwa mjumbe wa kamati ya maridhiano iliyoundwa mwishoni mwa kikao kupendekeza maazimio ya Bunge.
“Si kweli,” alisema waziri huyo wa nchi anayehusika na sera, utaratibu na Bunge.
“Unajua PAC walikuwa wanafanya kazi chini ya hazina. Hata Spika wa Bunge hakuiona hiyo ripoti, aliisikia tu ikisomwa bungeni. Kwanza kamati ilikuwa ikidurufu hiyo taarifa yake eneo la mbali na ili uipate ilikuwa ni lazima umrubuni Zitto.”
Aliongeza kusema: “Kama kweli nilikuwa nataka kuiba taarifa yao nisingekubali kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya maridhiano, iliyokutana kupitia upya mapendekezo ya PAC baada ya yale ya awali kuzua mvutano bungeni.”
Hata hivyo, Filikunjombe, ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa walilazimika kumwondoa eneo la kuchapishia ripoti hiyo. “Waziri Lukuvi alitumwa saa 9:00 usiku kuiba taarifa yetu wakati tunaichapa. Taarifa ilikuwa katika ‘flash’ na tulipogundua hilo tulimfukuza. Sisi tuliamua kuilinda ripoti ili isiibwe,” alisema Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa kwa tiketi ya CCM.
“Ile taarifa tuliichapa usiku wa kuamkia Jumatano ambayo ilikuwa siku ya kuiwasilisha bungeni. Na hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kikao cha Bunge kuahirishwa mara tu baada ya PAC kuwasilisha taarifa yake, ili Serikali ikajipange,” aliongeza.
Mbali na kauli yake ya jana, Filikunjombe aligusia suala hilo la ulinzi wakati akishukuru wabunge kwa kushikamana katika kufikia maazimio manane ya kuwawajibisha wote waliohusika.
Katika shukrani hizo, Filikunjombe alisema walilazimika kukesha usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita kuilinda ripoti yao isiibiwe na hivyo kuwashukuru watendaji wa Bunge kwa kazi nzuri.
Hata hivyo, kabla ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo kulienea taarifa kuna watu waliiiba na kunyofoa kurasa zilizokuwa na nyaraka za vielelezo na baadaye kuanza kuzisambaza. Polisi ilidai baadaye kuwa ilimkamata mtu aliyekuwa akisambaza vitabu hivyo vya ripoti, lakini hadi leo hajafikishwa mahakamani wala hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na polisi kuhusu maendeleo ya mtuhumiwa huyo.
Katika sakata hilo kubwa la aina yake, Bunge limtia hatiani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Mwanasheria Mkuu Jaji Fredrick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Eliachim Maswi na wakurugenzi wa Shirika la Umeme kwa kuhusika kwa makusudi au kwa uzembe katika kufanikisha miamala haramu kutoka kwenye akaunti hiyo.

AKODI MATARUMBETA KWENDA KUMSUTA MWIZI WA BWANA WAKE WA ESCROW


Makubwa! Wakati Wizara ya Nishati na Madini ikiwa kwenye msukosuko wa fedha zilizochotwa ‘kihuni’ kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, mwanaume mmoja, mtumishi wa wizara hiyo mkoani hapa almaarufu Kigogo wa Escrow, amesababisha wanawake wawili kusutana kwa matarumbeta na kukabana wakidaiwa kumgombea kwani ana fedha ‘chafu’.
Wakina mama, Tabu Mohamed na Mwajuma Chota  ( katikati ) wakisutana kwa kuibiana mabwana.
Tukio hilo la aina yake lilijiri wikiendi iliyopita katika Mtaa wa Karume mjini hapa ambapo wanawake hao, Tabu Mohamed na Mwajuma Chota walisababisha pakachimbika hadi polisi walipofika na kuokoa jahazi.
Awali ilifahamika kwamba wanawake hao walikuwa wakiishi pamoja maeneo ya Kikundi, Kata ya Sultan Area mkoani hapa. Kwa mujibu wa madai ya mashuhuda waliokuwa wamefunga mtaa huo, Tabu ndiye aliyeanza ‘kuchepuka’ na kigogo huyo ambaye ni mume wa mtu aliyemnunulia gari aina ya Toyota Opa.
Madai yaliendelea kushushwa kwamba, Mwajuma ambaye ni mke wa mtu alipoona mwenzake anakula vinono, naye akajiweka.
Bendi ilikodiwa na Tabu Mohamed ili kumsuta shosti yake Mwajuma Chota.
Habari za mtaani zilidai kuwa katika kujiweka, alifanikiwa kulamba mshiko wa shilingi elfu 80 kabla ya kushtukiwa na Tabu huku naye akitaka kuhongwa gari kama mwenzake.
Ilielezwa kwamba katika kufuatilia, Tabu aligundua kuwa Mwajuma anachepuka na ‘mshefa’ wake ndipo akapanga mashambulizi ya vita vya ardhini.
Kwa hasira, Tabu alishonesha sare za ‘madila’ na kununua mizinga ya pombe kali ambapo alienda kukodi matarumbeta na watu wa kusuta.
Wakubwa kwa watoto wakishuhudia vimbwanga vya wakinamama hao.
Ilisemekana kwamba kabla ya tukio, watu walipiga pombe kisha wakamfuata nyumbani kwao, Mtaa wa Karume na kulianzisha.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda ambalo liliwasili eneo la tukio ndani ya dakika sifuri juu ya tukio hilo, Mwajuma alifunguka: “Namshangaa Tabu kuja kunifanyia vurugu wakati na yeye ni mwizi tu. Huyo bwana ni mume wa mtu.”
Kwa upande wake, Tabu alidai Mwajuma ni shosti yake lakini alimtendea kitendo kibaya cha kutembea na bwana’ke.
Mmoja wa wamama hao, Tabu Mohamed  akichukuliwa na polisi kwa kumletea fujo mwenzake, Mwajuma Chota.
Alipobanwa zaidi hasa suala la kukodisha matarumbeta na kwamba mwanaume huyo ni mume wa mtu, Tabu alidai kwamba jamaa huyo alimkataza kuzungumza na wanahabari.
Baada ya kuipata ishu hiyo, gazeti hili liliwasiliana na mke wa kigogo huyo na kumuuliza kama ana habari kwamba kuna wanawake wanamgombea mumewe ndipo akapatwa na mshtuko na kuahidi kulifanyia kazi na kama ni kweli atafungasha virago.
Makamanda wa Polisi wakiimarisha ulinzi eneo la tukio.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Karume, Elly Mgota alithibitisha vurugu hizo kutokea kwenye mtaa wake ambapo sakata hilo lilitinga polisi baada ya Tabu kutiwa mbaroni kwa kosa la kumfanyia fujo mwenzake.

NAY WA MITEGO AFUNGUKA KUHUSIANA NA WIZI WA ESCROW


Haya ndo maneno ya Nay wa mitego kuhusiana na kashfa ya escrow

"Hii nchi imeozaa.Kwa Stahili hii viongozi wataendelea Kuiba tu. Coz wanajua hawatafungwa na wataendelea kubebana na Yataisha tu.

Nyie wananchi mnaojifanya mnahasira kwa kupiga wezi hamna lolotee. Wezi wa kupiga mnawaacha mnawapiga vibaka.

Ndio nyie mtu mweusi akiiba kitumbua mnampiga,akiiba
mzungu kitumbua hicho hicho mnaishia kucheka tu. Yani Hata nisikie nchi hii imeuzwa sitashtuka na wala sitahangaika kuangalia sijui bunge sijui uchafu gani. Yani ukipata nafasi ya kupiga hela nchi hii wewe piga tena kwa asilimia zote wala usiogope"

ORODHA YA WALIOTAFUNA FEDHA ZA ESCROW NA RIPOTI YA PAC HII HAPA


. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imewataja vigogo wa serikali, wanasiasa na viongozi wa dini watatu walionufaika na uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow na jinsi baadhi walivyotumia mifuko ya plastiki kuzibeba.
Akisoma maoni ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe aliwataja waliochukua fedha hizo kutoka kwa mkurugenzi wa VIP, James Rugemalira na kiwango walichopokea katika mabano kuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge (Sh1.6 bilioni) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka (Sh1.6 bilioni).
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (Sh40.4 milioni), aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4 milioni), Mbunge mstaafu wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh40.4 milioni), aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni).
Alisema majaji walioingiziwa fedha ni Jaji Profesa Eudes Ruhangisa (Sh404.25 milioni) na Jaji A.K Mujulizi (Sh40.4 milioni).
Kwa upande wa watumishi wa umma, Zitto alisema kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko (Sh40.4 milioni), aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Daniel Ole Naiko (Sh40.4 milioni) na ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lucy Appollo (Sh80.8 milioni).
Askofu Kilaini atajwa
Zitto alisema, “Kwa upande wa viongozi wa dini ambao waliingiziwa fedha na Benki ya Mkombozi ni Askofu Methodius Kilaini (Sh80.9 milioni), Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh40.4 milioni).
Aliongeza, “Kamati ya PAC ilithibitishiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru kuwa baadhi ya watu walienda kugawana fedha kwenye benki tajwa (Mkombozi) wakiwa na mifuko ya rambo, sandarusi, maboksi, magunia na lumbesa.”
Mkurugenzi Rugemalira
Zitto alisema Mkurugenzi Mtendaji wa VIP Engeneering, James Rugemalira alipata mgawo wa Dola za Marekani Sh75 milioni kutoka katika fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na kuzigawa kwa watu mbalimbali.
Rugemalira ambaye alikuwa na hisa 3 kati ya 10 za kampuni ya IPTL, alichukua kiasi hicho cha fedha na kukipeleka katika Benki ya Mkombozi inayomilikiwa na Kanisa Katoliki.
Zitto alisema Rugemalira alionekana kuhusika na IPTL pale alipofungua shauri mahakamani kuomba kuiondoa IPTL kwenye ufilisi na kisha kuuza hisa zake kwa kampuni ya PAP.

Alisema baada ya uamuzi wa Kahakama Kuu kutolewa Septemba 5, 2013, fedha za Escrow zilitolewa kwa haraka na kupelekwa katika benki hiyo baadaye kugawiwa kwa vigogo hao.
Kamati hiyo imekabidhiwa taarifa za Benki za Stanbic na Mkombozi ambazo zimeonyesha namna ambavyo fedha zilichukuliwa na watu na kampuni mbalimbali.
Ripoti hiyo ya PAC iliyosomwa jana ilikuwa na kurasa 116 na maneno 16,979.

ESCROW "WABUNGE WAGANYIKA"


Dodoma. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo jana alipangua hoja zilizotolewa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu ufisadi uliofanyika katika Akaunti ya Tegeta Escrow na kuacha wananchi njia panda kwa kutokuelewa nani anasema ukweli kati yake na kamati hiyo, inayoongozwa na Zitto Kabwe.
Juzi, kamati hiyo ya Zitto iliwasilisha ripoti yake kuwa imethibitisha kuwa Profesa Muhongo amekuwa mara kwa mara akilipotosha Bunge na Taifa kwa ujumla kwamba ndani ya fedha hizo hakukuwa na fedha za umma.
Kamati hiyo ilieleza kuwa imebaini kuwa Profesa Muhongo ndiye aliyekuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Singh Sethi na James Rugemalira tena katika ofisi ya umma na pengine hilo ndilo lilikuwa sababu ya upotoshaji.
Akiwasilisha taarifa ya Serikali kuhusu hoja hiyo, Profesa Muhongo alianza kupangua hoja moja baada ya nyingine ingawa katika mjadala wa baadaye, zilihojiwa na wachangiaji wengine waliohoji uhalali wa vielelezo alivyotoa.
Kutaifisha mitambo
Jana, alieleza kuwa pendekezo la Kamati ya PAC kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe si sawa kwa kuwa kulingana na mkataba wa PPA kati ya Tanesco na IPTL, majukumu ya IPTL yalikuwa ni kujenga, kumiliki na kuendesha (Build, Own and Operate – BOO). Hivyo, kutaifisha mtambo huo ni kukiuka makubaliano katika mkataba wa PPA wa Mei 26, 1995.
“Ukiukwaji wa aina hii ukitokea unaweza kuingiza Serikali katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwenye Mahakama za kibiashara za kimataifa. Aidha, utaifishaji wa miradi ya uwekezaji binafsi itakuwa ni njia ya kufukuza wawekezaji.”
Gharama za uwekezaji
Kuhusu taarifa ya kamati ya PAC kwamba mwaka 2004 Tanesco ilifungua shauri katika Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Kiuwekezaji (ICSID 2) kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya gharama za uwekezaji, Profesa Muhongo alisema suala hilo si kweli.
Alifafanua kuwa Tanesco haijawahi kufungua shauri lolote ICSID ya London au Mahakama yoyote dhidi ya Benki ya Standard Charterd kupinga kiasi kikubwa cha Capacity Charge kama inavyoelezwa na PAC.
“Shauri la ICSID 2 lilifunguliwa Oktoba 31, 2010 na Standard Chatered Bank Hong Kong (SCBHK) kwa ajili ya kudai malipo ya deni ililonunua kutokana na mkopo uliotolewa na mabenki ya ushirika ya Malaysia kwa IPTL. Wahusika katika shauri hilo la ICSID 2 ni SCBHK na Tanesco na wala siyo Tanesco na IPTL.”
Alisema Februari 12, ICSID ilitoa uamuzi kuhusiana na shauri la SCBHK na Tanesco na kuwashauri wakae kukokotoa upya malipo ya Capacity Charge. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kwa pande hizo kutekeleza uamuzi huo kutokana na pande hizo kutokuwa na mkataba wa kibiashara baina yao.
 Vilevile, kupitia shauri la madai Na. 60/2014, lililofunguliwa na IPTL katika Mahakama Kuu ya Tanzania Aprili 4, ilizuia utekelezaji wa maelekezo hayo,” alisema.
Uwekezaji wa Sh50,000
Profesa Muhongo alisema kuhusu madai ya PAC kuwa mtaji wa uwekezaji katika mtambo wa IPTL ni Sh50,000 na kwamba huo ndiyo ungetumika kukokotoa gharama za uwekezaji ili kulipa tozo ndogo kuliko ilivyo sasa, maelezo hayo siyo sahihi.
Alisema ukweli ni kwamba kutokana na uamuzi ya ICSID 1 ya Julai 12, 2001, gharama za ujenzi wa mtambo wa Tegeta ni Dola za Marekani 127.2 milioni kama ilivyoelezwa na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Profesa Muhongo alisema katika taarifa hiyo, pia imeelezwa kuwa ilikubalika kuwa uwiano wa deni na mtaji utakuwa 70:30 ikiwa na maana kwamba, deni ni Dola za Marekani 89.04 milioni na mtaji ni Dola za Marekani 38.16 milioni na kwamba uamuzi huo haujabadilishwa na Mahakama yoyote au mtu yeyote.
“Tunakubaliana kwamba fedha iliyopokewa kutoka mabenki ya ushirika ya Malaysia kama mkopo ni Dola za Marekani 85.86 milioni ambazo kati ya Dola za Marekani 105 milioni zilizokuwa zimeidhinishwa,” alisema na kuongeza:
“Swali la kujiuliza je, mtambo huo ulikamilikaje kwa gharama ya Dola za Marekani 85.86 milioni, huku gharama halisi ya ujenzi wa mtambo wa Tegeta ikawa Dola za Marekani 127.2 milioni?
Alisema ni dhahiri kwamba kuna matumizi ya zaidi ya Dola za Marekani 38.16 milioni ambazo pia zimetumika kwenye uwekezaji na kwamba Kamati ya PAC haikuonyesha fedha hizo kuwa sehemu ya uwekezaji.
PAP na umiliki wa hisa saba
Profesa Muhongo alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa za Brela za Desemba 31, 2013, uhamishaji wa hisa saba za Mechmar katika IPTL kwenda PAP ulisajiliwa hapa nchini. Kwa maana hiyo, PAP ni mmiliki wa asilimia 70 za IPTL.
Alisema Kamati ya PAC imeeleza kuwa PAP siyo mmiliki halali wa hisa saba za Mechmar katika IPTL lakini kamati imethibitisha kwamba nyaraka za mauziano kati ya Mechmer na Piper Link zilipokewa na Harbinder Singh Sethi ambaye pia ndiye mmiliki wa PAP.
“Kwa uthibitisho huo, kamati inakubali kuwa hisa za Mechmer katika IPTL zinamilikiwa na PAP,” alisema Profesa Muhongo.


Akana kuwa dalali
Profesa Muhongo alisema taarifa ya Kamati ya PAC kwamba yeye ndiye aliyekuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Harbinder Sethi na James Rugemalira siyo sahihi kuwa tangu Novemba 9, 2011, Rita iliitisha mkutano na kuwakutanisha wadau wote wa IPTL wakati yeye alikuwa hajateuliwa kwenye wadhifa huo.
“Mimi kama ni dalali, udalali wangu ni kupeleka umeme vijijini. Mimi kama ni dalali udalali wangu ni kusaidia wachimbaji wadogo wa madini na kupeleka Watanzania kusoma masters (shahada ya pili) duniani kote.”
Serikali kutokuchukua tahadhari
Waziri alisema Kamati ya PAC, imeeleza kuwa Serikali haikuchukua tahadhari ya kutosha dhidi ya madai mengine yanayoweza kujitokeza kabla ya kutolewa kwa fedha kutoka akaunti ya escrow kitu ambacho alidai si kweli.
Profesa Muhongo alisema kinga iliyochukuliwa inakidhi matakwa ya kisheria na imezingatia athari yoyote ambayo ingeweza kutokea baadaye kutokana na kutolewa kwa fedha katika akaunti ya escrow.
“Kwa hiyo, siyo kweli kwamba Serikali haikuchukua tahadhari kama ilivyodaiwa na PAC.”
Madai ya Sh321 bilioni
Profesa Muhongo alisema hoja ya PAC kwamba imejiridhisha kuwa madai ya Tanesco ya Sh321 bilioni yana uhalali japo usahihi wake utapatikana baada ya kutekelezwa kwa uamuzi wa ICSID 2 na Tanesco na IPTL kukubaliana kiwango sahihi cha Capacity Charge haina nguvu.
“Madai ya kwamba Tanesco inaidai IPTL Sh321 bilioni msingi wake ni dhana kwamba mtaji wa IPTL ni Dola za Marekani 100, sawa na Sh50,000 kwa wakati huo. Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba Dola za Marekani 38.16 milioni ziliwekezwa kwenye mradi wa Tegeta,” alisema.
Profesa Muhongo alisema Bodi ya Tanesco imekana kuyatambua madai hayo ya Sh321 bilioni... “Kimsingi hata vitabu vya hesabu vya Tanesco ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG, havionyeshi kuwapo kwa deni hilo.”

WAZEE WA "ESCROW" NGOMA NGUMU


WAKATI sakata la kuchukuliwa kwa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow likiendelea kuwa gumzo la sasa la mjini, sura mpya imeanza kujitokeza kwa watu zaidi wanaohusishwa na kugawiwa salio kutajwa, licha ya waliotajwa awali kuendelea kubakia katika orodha.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Kashfa hiyo iliibuliwa kwa mara ya kwanza na mbunge wa Kigoma Kusini kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila katika kikao cha Bunge lililopita, kitu ambacho kilipingwa kwa nguvu kubwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Hata hivyo, kadiri siku zinavyokwenda hali imeonekana kuwa ni ngumu kwa vigogo wa serikali kwani wanaonekana kama wameshikwa pabaya na wengi wametajwa kuhusika kwa njia moja au nyingine.
Ukiacha Werema, Muhongo na Eliakim Maswi kutajwa kunufaika na uchotwaji wa fedha hizo zilizokuwa Benki Kuu, wengine wanaodaiwa kupata mgao huo ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali, Andrew Chenge na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndullu.
4Aidha vigogo wengine wengi, wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, nao wanatajwa kuhusishwa na ukwapuaji wa fedha hizo kutokana na nyadhifa zao.
Lakini wakati Bunge hilo likianza vikao vyake vya wiki hii, Spika wa Bunge, Anne Makinda, naye alitajwa bungeni na Mbunge wa Mkanyageni kwa tiketi ya CUF, Habib Mnyaa kuwa anadaiwa kupewa mgao wa dola milioni moja za Marekani.
Kana kwamba haitoshi, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali, katika kijarida maalum kilichochapishwa kumchafua kilichosambazwa Dodoma, naye anatajwa kuchukua mlungula kutoka kampuni inayohusishwa na sakata hilo ya PAP.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kutunza fedha ambazo Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) zilipaswa kuilipa kampuni ya kufua umeme wa IPTL kwa kuiuzia nishati hiyo.
Hiyo ilitokana na shirika hilo la umma, kushtaki katika mahakama ya kibiashara ikilalamikia bei kubwa iliyotozwa na IPTL na kusababisha kufunguliwa kwa akaunti hiyo ili fedha hizo ziwekwe huko hadi muafaka baina ya pande hizo mbili utakapopatikana.
Hata hivyo, kabla ya muafaka huo kupatikana, wajanja walikwenda na kuzichukua fedha hizo ambazo sasa zinawatokea puani!

WAZIRI MKUU NA WASHIRIKA WAKE KUWAJIBISHWA, SAKATA LA ESCROW.



KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imependekeza kutenguliwa kwa nyadhifa na kuwajibika kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri kutokana na sakata la fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow ya Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.
Mbali ya mapendekezo hayo, Kamati hiyo imependekeza pia wote waliochukua fedha kutokana na kashfa hiyo iliyohusisha Sh bilioni 306, wafilisiwe mali zao na kushitakiwa mahakamani.

Wanaotajwa kutakiwa kutenguliwa kwa nyadhifa zao mbali ya kuwajibika kwa Pinda ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Naibu wake, Stephen Maselle, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliachim Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Kamati hiyo ilitoa mapendekezo yake hayo kutokana na matokeo ya ukaguzi maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akisoma maoni na mapendekezo ya Kamati baada ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe kusoma sehemu ya uchambuzi wa sakata hilo, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema kwa uzito na unyeti wa suala hilo, Waziri Mkuu Pinda anapaswa kuwajibika kwa kauli zake na kwa kutotekeleza wajibu wake wa kikatiba ipasavyo, ili kurejesha imani ya wananchi kwa Serikali yao na viongozi wao wa kisiasa.
Kwa mujibu wa Filikunjombe, baada ya kupitia vielelezo vilivyomo katika ripoti ya CAG, “Kamati imejiridhisha pasipo mashaka kuwa, Waziri Mkuu alikuwa na taarifa zote kuhusu mchakato mzima wa kuchotwa fedha kutoka katika akaunti ya Escrow.”
“Ushahidi ulioletwa na Ofisi ya CAG kwenye Kamati unaonesha kuwa Waziri Mkuu alikuwa akipata taarifa za jambo hili. “Na Kamati imesikitishwa kuona kuwa Waziri Mkuu hakuchukua hatua zozote kuzuia muamala huu usifanyike,” aliongeza Makamu Mwenyekiti huyo, na kubainisha kuwa Pinda pia aliwahi kunukuliwa akisema fedha za Escrow si za umma.
Kuhusu Profesa Muhongo, Kamati ilieleza kuwa alifanya udalali wa kuwakutanisha Harbinder Sethi na James Rugemalira (waliokuwa wamiliki wa Independent Power Tanzania Limited) na kuwa alilipotosha Bunge kuhusu fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kwamba ndani ya fedha hizo, hakukuwa na fedha za umma.
“Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, aidha kwa makusudi, ama kwa sababu anazozijua vizuri zaidi mwenyewe, Waziri wa Nishati na Madini ananukuliwa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge, kwa nguvu kubwa na kwa kujiamini, akitetea uchotwaji wa fedha hizo kinyume cha masharti ya mkataba wa Escrow,” alisema Filikunjombe.

Alisema iwapo waziri huyo angetimiza wajibu wake kidogo tu na ipasavyo, fedha za Tegeta Escrow zisingelipwa kwa watu wasiohusika na nchi ingeweza kuokoa mabilioni yaliyopotea kama Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Capital Gain Tax na ushuru wa stempu ambazo ni sawa na takribani Sh bilioni 30.
“Kamati inapendekeza kuwa mamlaka yake ya uteuzi, itengue uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini kutokana na sababu zilizoelezwa,” alisema.

Akimzungumzia Maselle, Filikunjombe alisema Kamati imethibitisha kuwa alisema uongo bungeni kwa kutamka kauli ambazo zilikuwa na lengo la kupotosha umma kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow, ikiwemo kutoa kauli ambazo zingeweza kusababisha nchi kuingia kwenye mgogoro wa kidiplomasia na nchi ya Uingereza.

“Kamati inapendekeza kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini) achukuliwe hatua kali za kinidhamu, ikiwemo kutenguliwa uteuzi wake. “Kamati pia inapendekeza kuwa Naibu Waziri huyu afikishwe mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili ili aadhibiwe kama mbunge kwa kusema uongo bungeni ili liwe fundisho kwa wabunge wengine kuhusu kauli wanazotoa ndani ya Bunge lako tukufu,” aliongeza Filikunjombe.

Kuhusu Mwanasheria Mkuu Jaji Werema, Kamati ilisema imethibitisha kuwa alitoa ushauri ulioipotosha Benki Kuu ya Tanzania kuhusu hukumu ya Jaji John Utamwa kwa kutumia madaraka yake vibaya.
Alisema Jaji Werema aliagiza kodi ya Serikali yenye thamani ya Sh bilioni 21 isilipwe na hivyo kuikosesha Serikali mapato adhimu.

“Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kujua na kwa makusudi alilipotosha Bunge na Taifa kwamba mgogoro uliosababisha kufunguliwa kwa akaunti ya Escrow ulikuwa ni mgogoro wa wanahisa wa IPTL badala ya mgogoro kati ya Tanesco na IPTL.“
Kamati inapendekeza kuwa uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali utenguliwe na mara moja afikishwe mahakamani kwa matumizi mabaya ya ofisi yaliyosababisha Serikali kupoteza mabilioni ya fedha,” alisema Filikunjombe.

Akimzungumzia Katibu Mkuu Maswi, Makamu Mwenyekiti huyo wa PAC alisema Kamati inapendekeza uteuzi wake utenguliwe na Takukuru wamfikishe mahakamani mara moja, kwa kuikosesha Serikali mapato na matumizi mabaya ya ofisi na kusaidia utakatishaji wa fedha haramu.
Kamati ilisema imethibitisha Maswi amefanya uzembe wa hali ya juu wa kushindwa kujiridhisha kuhusu masharti ya sheria ya kodi, na pia imebaini kuwa hakujiridhisha uhalali wa Kampuni ya Mechmar kuuzwa kwa Piperlink na baadaye kuuzwa kwa PAP, na hivyo kusababisha fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kulipwa kwa asiyestahili kinyume cha mkataba wa akaunti ya Escrow.

Source: Habari Leo.

CHIEF KIUMBE" ADAKWA NA POLISI MKOANI DODOMA



Inasadikika Chief Kiumbe yupo lupango Dodoma kwa makosa mawili moja kukutwa na nyaraka za bunge isivyo halali, mbili kutumia vijana kutishia wajumbe wa kamati ya PAC kwa maelekezo ya Waziri wa Nishati na madini Bw Pro.f Muhongo.

Ni bahati mbaya ila ukweli ni kwamba Muhongo, Werema, na Maswi ni maswahiba wa kutoka sehemu moja ya nchi na hivyo kujikuta wakitumia vijana wao wa kazi kudhibiti anguko lao.

Wizi huu ni wa aibu sana kwa taaluma zao na watu wao. Inasadikika chief Kiumbe aliwahi ama bado ni jambazi hasa pale ambapo rafiki yake ambaye siku zote chief anamkumbuka sana aliuwawa kwa risasi kwenye tukio la ujambazi.

Ni ripoti kutoka Dodoma ni mimi

Chief Mkwawa- mpaka hapo baadaye kwenye saga la ESCROW- hakuna kuzuia mafuriko kwa viganja.
Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

Majanga