Hati za viapo hivyo zinathibitisha kwamba Mandela anapumua kwa mashine na madaktari wanaomtibu waliishauri familia kuondoa mashine hizo suala ambalo limebaki katika mikono ya familia. Viapo hivyo viliandikwa Juni 26 mwaka huu na kuwasilishwa mahakamani Juni 28, lakini havikuwahi kutolewa hadharani hadi Julai 3, wakati uamuzi wa kesi ulipotolewa na kumwamuru mjukuu wa Mandela, Mandla arejeshe mabaki ya miili ya watoto wa babu yake Qunu. Mabaki hayo yaliyohamishiwa Mvezo 2011 ni ya watoto wa Mandela ambao ni Madiba Thembekile aliyefariki kwa ajali ya gari 1969, Makgatho aliyefariki 2005 na binti yake wa kwanza Makaziwe (mkubwa) aliyefariki dunia 1948 akiwa mtoto mchanga.
Mabaki hayo yalizikwa juzi Alhamisi katika makaburi ya familia, Qunu ikiwa ni utekelezaji wa amri ya mahakama. Kati ya juzi na jana, Ikulu ya Pretoria ililazimika kutoa taarifa mbili; moja muda wa jioni na nyingine usiku wa kuamkia jana ikiwa ni hatua ya kuondoa hofu iliyokuwa imeanza kusambaa baada ya vyombo vya habari kuweka bayana kilichoandikwa katika viapo vya mahakama. Hoja kubwa ambayo imekuwa ikijadiliwa ni kwa jinsi gani viapo vya mahakama vionyeshe kwamba uwezekano wa Mandela kuendelea kuishi ni mdogo huku Serikali ikitoa taarifa kwamba hali ya Mandela ni imara licha ya kwamba yu mahututi. Katika taarifa zote mbili Rais Jacob Zuma kupitia kwa msemaji wake, Mac Maharaj aliweka wazi kwamba Mandela ‘siyo mtu wa kufa wakati wowote’ kama ilivyoripotiwa ikasisitiza kwamba hali yake imeendelea kuwa imara licha ya kwamba ni mgonjwa sana.
Source: Mwananchi.