Saa chache kabla ya kuanza kwa tukio maalumu la kihistoria la Ibada ya Kitaifa ya kumuaga Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, makomandoo wa Marekani wameshika jukumu la ulinzi katika maeneo nyeti nchini hapa. Ulinzi huo unatokana na ujio wa Rais wa Marekani, Barrack Obama, mkewe Michelle pamoja na viongozi wa nchi mbalimbali, ambao watahudhuria tukio linalotarajiwa kushuhudiwa na mamilioni ya watu; ndani na nje ya Afrika Kusini.
Rais Jacob Zuma atahutubia katika ibada hiyo, ambayo itafanyika katika Uwanja wa FNB (Soccer City), wenye uwezo wa kuchukua watu 95,000 kwa wakati mmoja.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano ya Afrika Kusini inasema milango ya uwanja huo ambao ulitumika wakati wa sherehe za ufunguzi na fainali za Kombe la Dunia 2010, itakuwa wazi kuanzia saa 12:00 na Ibada ya kwaheri inatarajiwa kuanza saa 5:00 asubuhi.
Karibu barabara zote za kuingia uwanjani hapo zimetangazwa kufungwa kwa ajili ya magari yote, badala yake Serikali imeandaa usafiri wa bure kwa wananchi watakaokwenda katika tukio hilo.
Jana, kutwa nzima, helikopta zilikuwa zikiruka katika anga la Jiji la Johannesburg lakini zilitumia muda mwingi zaidi kuzunguka juu ya Uwanja wa FNB ulioko Soweto, huku kukiwa na taarifa kwamba makomandoo wa Marekani walikuwa kazini, kuhakikisha usalama wa kiongozi wao.
Pamoja nao, mamia ya polisi wa Afrika Kusini walionekana katika maeneo yanayozunguka uwanja huo, huku baadhi ya vyombo vya habari vikiwanukuu maofisa wa Serikali kwamba askari 11,000 watashiriki katika ulinzi wakati wa maombolezo na mazishi.
Ulinzi pia umeimarishwa katika sehemu mbalimbali za Jiji la Johannesburg pamoja na kule atakakozikwa katika Kijiji cha Qunu, Mthatha ambako wanajeshi wenye silaha wamelizunguka eneo la makazi ya kiongozi huyo.
Maeneo mengine yaliyowekewa ulinzi mkali ni katika viwanja vya ndege na katika Majengo ya Umoja (Union Buildings) jijini Pretoria ambako mwili wa Mandela utawekwa kwa ajili ya wananchi kutoa heshima za mwisho kati ya keshokutwa na Ijumaa.
Vituo vya televisheni vya Afrika Kusini vilionyesha magari ya kijeshi zaidi ya 10 yakiwa yameegeshwa katika eneo linalozunguka makazi ya Mandela, Qunu.
Waandishi waliokuwa wamepiga kambi karibu na makazi ya Mandela, Qunu walihamishwa na kuwekwa mbali zaidi kutokana na sababu walizoelezwa kuwa ni za kiusalama.