Siku moja baada ya kuwasilisha maelezo yake ya utetezi baada ya kuvuliwa nyadhifa zake ndani ya Chadema, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe amekata rufaa Baraza Kuu kupinga hatua hiyo.
Zitto pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo walivuliwa nyadhifa zao na Kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Novemba 20 na 21 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana, Mwanasheria wa Zitto, Albert Msando alitaja sababu mbili za kukata rufaa kuwa ni kukiukwa kwa taratibu za kuchukua hatua za nidhamu na sababu zilizotolewa kutokuwa sahihi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema mambo hayo yalishatolewa ufafanuzi na chama na kwamba kukata rufaa ni haki ya kikatiba kwa mwanachama yeyote.
“Kukata rufaa ni haki ya kikatiba ya wanachama yeyote. Rufaa ikatwe tu, itashughulikiwa kwa mujibu wa katiba, kanuni, maadili na itifaki ya chama. Hata hivyo, ieleweke, rufani inahusu kuvuliwa nafasi za uongozi, kusudio hilo haliwaondolei wajibu wa kujieleza kwa maandishi mbele ya Kamati Kuu kwa nini wasifukuzwe uanachama,” alisema Mnyika.
Sababu za kukata rufaa
Akifafanua sababu za kukata rufaa, Msando alitaja kifungu cha 6.5.6 cha Kanuni ya Uendeshaji ya chama hicho, akisema utaratibu uliotakiwa kufuatwa kabla ya kumchukulia hatua za kinidhamu kiongozi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni ni kupewa kwanza mashtaka kwa maandishi ili apate nafasi ya kujibu.
“Kiongozi yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu bila kwanza kupewa mashtaka yake kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi ya kujibu mashtaka kwa maandishi,” alisema na kuongeza:
“Kwa mujibu wa ibara ya 5.4.3 na 5.4.4 ya Katiba mwanachama yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa ama kuachishwa ama kufukuzwa uanachama bila kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili.”
Alitaja vipengele vingine ni kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao kinachohusika na atajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao ndani ya wiki mbili baada ya kusikilizwa.
Hata hivyo, kipengele ‘d’ kinasema: “Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura bila kuzingatia utaratibu (b), (c) hapo juu kama itaona masilahi ya chama kwa ujumla yanaweza kuathiriwa isipokuwa mwanachama au kiongozi anayelalamikiwa atalazimika kuitwa kwenye kikao husika.
Alifafanua kuwa, siku ya kikao cha Kamati Kuu, Zitto hakupewa mashtaka yake bali aliyakuta ndani ya kikao baada ya kupewa taarifa kwa ujumbe wa simu (text message au sms). Zitto hakuwepo katika mkutano wa jana na waandishi wa habari.
“Kwa uzito wa makosa hayo yaliyosababisha kuvuliwa uongozi na kwa kuangalia athari zake kwake yeye binafsi na chama kwa jumla, Kamati Kuu ilitakiwa kujiridhisha kwamba kanuni za uendeshaji na katiba zinafuatwa,” alisema.
Mbali na Zitto, Msando alisema makosa hayo pia yalifanyika kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba. “Yeye hakuitwa kabisa kwenye kikao hicho na ni ukiukwaji wa Kanuni ya Uendeshaji 6.5.6(d),” alisema.
Aliongeza kuwa hata waraka wa mabadiliko ulioelezwa kuwa sababu ya Zitto kupewa adhabu hiyo haumtaji kabisa.
Akieleza nia ya Zitto kukata rufaa, Msando alinukuu katiba ya chama hicho ibara 6.3.6(d) na ibara 6.3.6(e) akisema:
“Kiongozi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu anayo haki ya kukata rufaa ngazi ya juu ya ile mamlaka yake ya nidhamu na uamuzi wa ngazi hiyo utakuwa wa mwisho”,” alisema na kuongeza:
“Huo ndio utaratibu ambao Zitto Kabwe ameamua kufuata kwa kuheshimu maamuzi ya Kamati Kuu lakini kukatia rufaa maamuzi hayo. Kuheshimu maamuzi siyo kuyakubali uhalali wake.”
Akana kuhujumu ziara ya Dk Slaa Kigoma
Katika hatua nyingine Msando alisema kuwa matukio ya vurugu yanayoiandama ziara ya Katibu Mkuu wa chama hicho mkoani Kigoma hayana uhusiano wowote na Zitto.
“Zitto Kabwe hahusiki kwa njia yoyote na hayo yanayoendelea na anayakemea na kuwashauri wanachama wote kuwa watulivu na kuendelea kuwaheshimu viongozi wa kitaifa,” alisema Msando.