Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limeomba kuongeza bei ya umeme kwa asilimia 67.87 ikiwa ni kutoka Sh197.8 kwa Unit mpaka Sh332.06.
Hayo yamebainishwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alipokuwa akiwasilisha maombi ya shirika hilo mbele ya Wadau wa Umeme na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).
Alisema kwa sasa uzalishaji wa umeme utokanao na nguvu za maji ni asilimia 13, utokanao na gesi ni asilimia 42 na utokanao na mitambo ya mafuta ni asilimia 45.
“Kutokana na kuongezeka kwa gharama za kutoa huduma, wastani wa bei iliyopo ya Sh197.8 kwa uniti, hailingani na wastani wa Sh332.06 kwa unit inayotakiwa kukidhi mahitaji ya sasa,” alisema Mramba na kuongeza:
“Hii ni pungufu kwa kiasi cha Sh134.25 kwa uniti, ongezeko la bei la asilimia 67.87 litafidia upungufu huo,” alisema Mramba.
Alisema, asilimia ya mapato yanayotumika kulipia gharama za umeme utokanao na mitambo ya dharura na ile ya binafsi ni asilimia 85. “Ikiwa ombi la ongezeko la bei ya umeme halitaridhiwa, shirika litashindwa kumudu gharama za uendeshaji na hivyo kutokidhi mahitaji makubwa ya umeme nchini na kutoa huduma zenye ubora unaokubalika kimataifa,” alisema Mramba.
Alisema madhara mengine yatokanayo na kutoongezwa kwa bei hiyo ni shirika hilo kutokidhi mikataba iliyoingiwa jambo alilosema litasababisha mgogoro ya kimikataba.
Mramba alieleza pia kuwa, hali hiyo italifanya shirika hilo kushindwa kulipa mikopo yake benki na kuathiri uwezo wake wa kuwekeza kupitia mikopo mipya.
Aliongeza kuwa, katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2013 matumizi ya umeme yamekuwa yakiongezeka wakati kiwango cha mvua kikiwa chini ya wastani hali iliyosababisha Tanesco kutumia zaidi umeme unaozalishwa kwa mafuta.
“Katika kipindi hiki kiwango cha gesi asili hakikukidhi mahitaji ya nishati kwa sababu ya ufinyu wa miundombinu ya gesi iliyopo. Upungufu huu ulisababisha mgawo wa umeme mwaka 2010 na 2011,” alisema na kuongeza:
“Athari ya mgawo wa umeme katika taifa ni kubwa, kulingana na utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia, hasara kwenye uchumi wa taifa ya kutokuwapo kwa umeme kutokana na mgawo ni wastani wa dola za Marekani 1.1 kwa kila uniti,”.
Katika hatua nyingine, Mramba alisema kutokana na gharama za uzalishaji kupanda, hasara ndani ya shirika hilo imeongezeka kutoka Sh43.43 bilioni mwaka 2011 hadi Sh178.45 bilioni mwaka 2012.