Beautiful Onyinye, Wema Sepetu ‘Madam’.
KIMENUKA!  Beautiful Onyinye, Wema Sepetu ‘Madam’ amemporomoshea matusi mazito  shemeji wa Zarina Hassan ‘Zari’, King Lauwrance akidai amemuudhi sana  kwa kitendo cha kuvujisha picha inayomuonesha akiponda raha nchini  Afrika Kusini ‘Sauz’ na mume wa Zari, Ivan Semwanga, Risasi Mchanganyiko  linakupa mchapo kamili.
Mwishoni  mwa wiki iliyopita, Wema na staa wa Bongo Fleva, Omari Nyembo ‘Ommy  Dimpoz’ walikwenda Sauz kurekodi video ya wimbo wa msanii huyo ambao  jina lake bado halijafahamika mara moja ndipo baadae picha ya Ivan, Wema  na King Lawrence ilipovuja na kuzua gumzo.
Kwa  mujibu wa chanzo chetu kilichokuwa Sauz, baada ya Wema na Ommy kutua  nchini humo na ‘project’  hiyo ya video, King Lawrance alidaiwa kuandaa  mpango kabambe wa kuhakikisha kwa namna yoyote wanaonana na Wema kisha  kupiga naye picha ambayo akiivujisha mtandaoni kila mtu ataamini  wamefanya malipizi kwa zilipendwa wa Wema, Nasibu Abdul ‘Diamond’ ambaye  amemnyakua Zari, mke wa Ivan.
“Ilikuwa  ni mpango wa malipizi, King na Ivan walikuwa wanaumia moyoni kumuona  Diamond anatoka na Zari wakati wao wana fedha kuliko Diamond hivyo  waliposikia mtoto wa kike (Wema) yupo Sauz wakasema watadili naye hadi  kieleweke, iwe ni kwa kufanikisha zoezi la kutoka naye kimapenzi au hata  kupiga picha ambazo zikisambaa mitandaoni, watu watajua kwamba  wamefanya malipizi,” kilisema chanzo chetu.
