Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema,Dk Willibrod Slaa amesema  Tanzania haiwezi kuendelea kuwa na amani kama wizi wa rasilimali za  taifa utaendelea.
Dk Slaa aliyasema hayo Dar es Salaam jana, wakati  alipofungua mkutano wa Bodi ya Kimataifa ya Shirikisho la Vyama vya  Kidemokrasia kwa Vijana (IYDU) ambao unafanyika kwa mara ya kwanza  katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Amani inakuwapo mahali penye haki” alisema Dk  Slaa na kutolea mfano wa askari ambao wamekuwa wakikamatwa na nyara za  taifa wakati wao ni vyombo vya dola, huku pia akisema migogoro ya ardhi  inayokithiri inaweka rehani amani ya taifa hili.
Haki nyingine alizolalamilia Dk Slaa ni pamoja na  kuminywa kwa demokrasia ambapo ametolea mfano wa polisi kuzuia mikutano  ya Chadema huku akiwatuhumu kuwa wamekuwa mashabiki wa siasa badala ya  kutimiza wajibu wa kulinda amani kwenye mikutano hiyo.
Kuhusu msajili wa vyama vya siasa John Tendwa, Dk Slaa alisema Chadema walishamfuta kwenye orodha ya watu wanaowasiliana nao.
Akizungumzia mpango wa chama hicho kuanzisha  kikosi cha ulinzi, Katibu huyo alisema hata kwenye majumba ya kawaida  watu wanakuwa na walinzi wao iweje wao kama chama wasifanye hivyo.
“Kuna walinzi wengi tu wanalinda majumba ya watu mjini, ni sheria gani inayotukataza sisi?” alihoji Dk Slaa.
Kwa upande wa ajira alisema, hakuna nchi inayoweza  kuwa na uchumi imara kama vijana wake hawana ajira. Naye Mwenyekiti wa  IYDU, Aris Kalafatis alisema ujumbe wao mkubwa kwa vijana wa Tanzania ni  kutaka mabadiliko hususan katika masuala ya maendeleo,huduma za jamii  na ukosefu wa ajira.
Akizungumzia migogoro mingine inayotokea katika  mataifa kama Misri na Tunisia, Kalafatis alisema hawaungi mkono kudai  haki kwa njia za machafuko, wanachohitaji ni kuona migogoro inatatuliwa  kwa njia za mazungumzo na siyo kama hali ilivyo sasa.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
