Dar es Salaam. Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), imesema matumizi ya chupa za plastiki za kunyonyeshea watoto maziwa, zinaweza kuwasababishia ugonjwa wa saratani.
Mratibu wa watoto wachanga na wadogo wa TFNC, Neema Joshua, alisema juzi kuwa taasisi hiyo inawataka wanawake kutumia vikombe badala ya chupa.
Joshua alisema chupa hizo zikioshwa kwa maji ya moto hutoa chembechembe, ambazo watoto wakizinywa zinaweza kuwasababishia ugonjwa huo, kwa maisha ya baadaye.
Alisema ingawa hakuna utafiti uliofanywa kuthibitisha hilo, lakini chembechembe za plastiki zinapotumiwa na binadamu huweza kusababisha saratani.
“Tunaomba wanawake wasitumie chupa hizo licha ya kuwa zipo nyingi dukani, watumie vikombe kuwanywesha watoto wao,” alisema.
Pia, Joshua alisema chupa hizo hazifai kwa sababu ni vigumu kuziosha kwa ufanisi, kutokana na muundo wake hali inayoweza kuwasababishia watoto magonjwa mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe, Dk Joyceline Kaganda, alisema ukosefu wa lishe bora unaweza kusababisha kudumaa kwa mwili hata akili.
“Tunaweza kulaumu Serikali kwa matokeo mabaya ya mitihani, lakini kumbe matokeo hayo yanaweza kusababishwa na ukosefu wa lishe kwa wanafunzi,” alisema. Dk Kaganda alitaka wanawake kuwanyonyesha watoto maziwa tangu wanapozaliwa hadi wanapofikisha umri wa miezi sita, bila kuongezewa chakula chochote.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Donald Mmbando, alisema ni asilimia 49 ya wanawake wanaojifungua ndiyo wanaowanyonyesha watoto kwa muda sahihi.
Chanzo:- Mwananchi