Mtwara/Dar. Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),  mkoani Mtwara wanadaiwa kuwakamata vijana wanne na kuwapeleka  kusikojulikana juzi jioni kisha jana kuwafikisha Kituo cha Polisi Mkoa  wa Mtwara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa  alikiri kukamatwa kwa watu hao: “Ni kweli tunawashikilia na tunahoji  pande hizo mbili; yaani wananchi na wanajeshi kujua ukweli uko wapi.”
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano  wa JWTZ, Meja Eric Komba alisema hana taarifa hizo... “Kama ni kuteka  JWTZ haliteki wananchi na kama ni kukamatwa, mimi sina taarifa ya  maandishi wala ya mdomo, ndiyo kwanza nasikia kwako. Nitafute kesho  nitakuwa nimeshafuatilia.”
Akizungumza kwa simu jana, Naibu Katibu Mkuu wa  CUF, Julius Mtatiro alisema tukio hilo lilitokea juzi saa kumi na moja  jioni wakati vijana hao pamoja na watu wengine walipokuwa wakiangalia  Kongamano la Amani nchini lililokuwa likirushwa moja kwa moja na Kituo  cha Televisheni cha ITV.
“Makundi ya wananchi yalikuwa yanafuatilia  kongamano pale Mtwara. Wale vijana walikuwa kwenye grocery iitwayo  Kwatelela inayotazamana na lango kuu la Mamlaka ya Bandari.  Walishangilia kwa nguvu kuunga mkono baadhi ya hoja zilizotolewa kwenye  kongamano. Karibu yao alikuwapo askari wa jeshi aliyevalia kiraia ila  hawakujua hilo,” alisema Mtatiro na kuongeza:
“Kongamano lilipokaribia kwisha, askari yule  aliwatolea bastola na kuwaweka chini ya ulinzi. Alipiga simu kuwaita  wenzake na mara gari la jeshi lilifika wakachukuliwa.”
Mtatiro alisema amepata taarifa hizo baada ya kupigiwa simu na mashuhuda wa tukio hilo juzi jioni.
“Nimezungumza na mashuhuda wanne ambao wao  wamenusurika baada ya kuwa mita chache katika eneo la tukio.” Mtatiro  aliwataja vijana hao kuwa ni Ismail Nduva, Boniface Mkamale, Ismail  Namwindula na Rashid Mniyanda.
Katika kongamano hilo ambalo lilihudhuriwa na  wasomi, wanasiasa na viongozi akiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk  Emmanuel Nchimbi,
Serikali ilitupiwa lawama katika masuala  mbalimbali hasa utendaji wa Jeshi la Polisi lakini pia Katibu Mkuu wa  Chadema, Dk Willbrod Slaa alilinyooshea kidole JWTZ kutokana na  kuandamwa na tuhuma za utesaji na ubakaji huko Mtwara.
Hata hivyo madai hayo yalipingwa vikali na  Brigedia Jenerali Elias Athanas aliyekuwapo katika kongamano hilo  akisema: “Naomba kuweka wazi kuwa jeshi letu huko Mtwara, lina adabu na  vitendo ambavyo vimekuwa vikiripotiwa ni vya propaganda tu kama  alivyosema Dk Slaa.”
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi
