Dar es Salaam. Serikali imesema suala la matumizi ya mafuta ya ubuyu sasa inawaachiwa wananchi wenyewe kutumia ama kuacha.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, alisema hayo jana alipotoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa mafunzo ya wataalamu kutoka vitengo vya mbalimbali vya Udhibiti Dawa na Chakula visivyofaa kwa matumizi ya binadamu kutoka nchi 16 za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwa kipindi cha mwezi sasa, watu mbalimbali kupitia vyombo wamekuwa wakitoa maoni ya kupinga kauli za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwamba mafuta hayo yana madhara kwa binadamu.
Dk Rashid alisema suala la mafuta ya ubuyu ni kwamba mlaji anapaswa kuwa na tahadhari hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuzuia vitu ambavyo vina madhara na vinavyoweza kusababisha athari kama saratani na magonjwa mengine.
“Mafuta ya ubuyu yana athari kama vitu vingine vyote vinavyokuwa na madhara kwa binadamu ila watu wanapaswa kujua kuwa madhara haya ni sawa na madhara ya mtu anayevuta sigara, licha ya tahadhari kuwekwa kuwa uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya hivyo hivyo hata kwa mtumiaji wa mafuta ya ubuyu madhara yapo na yameshadhibitishwa na TFDA hivyo ni jukumu la jamii kuzuia tatizo hilo” alisema Dk Rashid.
Jana hiyo gazeti moja linalochapishwa kila siku liliwanukuu watalaamu wa Hospitali ya Ocean maarufu kwa kutibu saratani kwamba hawajaona kansa inayoweza kutajwa kwamba ilisababishwa na mafuta ya ubuyu.
Lakini Naibu Waziri alisisitiza kwamba licha ya kuwapo kwa taarifa kuwa mafuta hayo hayana madhara, lakini TFDA wamepima na kugundua madhara kwa mtumiaji, hivyo jukumu hili ni la kila mmoja kuhakikisha kuwa anaacha kutumia mafuta hayo au anaendelea.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, kusema kuwa mafuta ya ubuyu hayana madhara yoyote katika mwili wa binadamu kama yakitumiwa vizuri.
Chanzoo: Mwananchi.
Chanzoo: Mwananchi.