Rais Jakaya Kikwete amesema amepata wakati mgumu alipouona mwili wa Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, alipokwenda kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo.
Rais Kikwete alikuwa miongoni wa marais na wageni wengine mashuhuri waliopewa nafasi za kwanza kutoa heshima za mwisho kwa Mandela, juzi katika Ikulu ya Pretoria ambayo iko katika Majengo ya Umoja (Union Buildings).
“Ni vigumu kufikiria kwamba nilichokiona ni kweli….kumwona Mzee Mandela akiwa amelazwa katika jeneza ni ngumu sana kuamini, nimepata wakati mgumu sana,” alisema Rais Kikwete kwa kusitasita huku akionekana mwenye sura ya huzuni.
Rais alikuwa akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Afrika Kusini (SABC) baada ya kutoa heshima za mwisho kwa Mandela.
Kikwete ambaye pia aliungana na viongozi wengine katika ibada ya kitaifa katika Uwanja wa FNB, Jumanne, aliondoka kurejea Tanzania juzi baada ya kutoa heshima za mwisho.
Kwa upande wake Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe alisema Mandela alikuwa mwanamapinduzi mwenzake na kifo chake ni pigo kubwa kwa wanamapinduzi wa Afrika.
“Tulisafiri katika barabara moja, tulibeba mizigo inayofanana; ambayo ni kuumizwa na kuongoza watu wetu, yeye kwangu alikuwa kaka na mkubwa wa umri, tumempoteza na tutamkumbuka,”alisema Mugabe.
Viongozi wengine wa Afrika ambao walihojiwa na SABC walimzungumzia Mandela kama mwalimu aliyewafunza somo la uongozi ambalo hawapaswi kuliacha kwa ajili ya wananchi wao na Bara la Afrika kwa jumla.
Rais wa Malawi, Joyce Banda yeye alisema: “Ni mwalimu ambaye alitufunza somo la uongozi, tunapaswa kuhakikisha kwamba tunalizingatia kwa ajili ya kuwaendeleza watu wetu ambao wanakabiliwa na matatizo mengi.”
Aliongeza: “Mandela alipigania elimu na hili ni jambo muhimu kwa nchi zetu na vizazi vya sasa, tunapaswa kuyapa kipaumbele mambo haya na mengine mema aliyotufunza”.
Rais Mstaafu wa Ghana, Jerry Rawlings alisema Mandela alikuwa na mamlaka ya mambo yote aliyokuwa akiyazungumza na kuwaasa Waafrika na dunia kwa kuwa alikuwa ni mtu wa vitendo.
“Alikuwa mtu mwenye sifa hizo na hakuwa mmoja wetu ambaye angempa changamoto kwamba anasema asichotenda, huu ni mfano ambao sisi viongozi wa sasa tunapaswa kuufuata,” alisema Rawlings.
Juzi mchana, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alimweleza Mandela kuwa kiongozi ambaye alikuwa na uwezo mkubwa katika majadiliano na kwamba uamuzi wake wa kukaa meza na makaburu haukukubaliwa na wahafidhina wengi ndani ya chama chake cha ANC.
Akiwahutubia wageni mashuhuri waliofika kutoa heshima za mwisho, Zuma alisema: “Oliver Tambo hakuwa tena na afya njema, hivyo hakutaka tena kugombea uongozi wa ANC hivyo Mandela alichaguliwa kuwa Rais.”
Alisema Mandela aliiongoza ANC katika majadiliano yaliyokuwa magumu baina yao na utawala wa Makaburu, lakini hatimaye kiongozi huyo alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza Mzalendo. “Alifanya jambo ambalo sisi wafuasi hatukuwahi kulifikiria kabla,” alisema.
Mwananchi.