KATIKA toleo namba 859 la Desemba 29 hadi Januari 2, 2014 la gazeti hili, kwenye safu yetu hiihii, niliandika kuhusu Snura Mushi, msanii anayetingisha anga la muziki wa mduara. Yupo juu kwa kuwa kibao chake cha Majanga kinasumbua mno hivi sasa.
Kwa wale ambao hawakubahatika kunisoma, niliandika nikionyesha masikitiko yangu kwa namna binti huyu anavyocheza akiwa jukwaani na hata kwenye video zake.
Kama haujawahi kumuona akiwa jukwaani, ni kwamba Snura anajua hasa kukichezea kiuno chake, ni mjuzi wa kukizungusha kwa namna ya kuburudisha kabisa na hatari zaidi, pale anapoamua kuwapa mgongo mashabiki walio ukumbini, kisha akawatingishia kwa namna ya kutetemesha makalio yake makubwa!
Ni aina ya uchezaji ambao kwa watu wazima, ni burudani mno, hasa kama wakati huo, tayari wale wa kiburudisho wanakuwa wamepata moja mbili. Uchezaji wake unaleta mfadhaiko zaidi hasa kutokana pia na uvaaji wake. Amechagua kuwa mtu mwenye mavazi tatanishi.
Lakini kama baba au mama waliostaarabika, hawawezi kujisikia vizuri kumuona msichana huyu akiwajibika jukwaani wakiwa na watoto wao, bila kujali kama ni wasichana au wavulana. Ni aibu, kinyume cha maadili na tena, hamna chochote ambacho watoto wadogo wanaweza kujifunza.
Katika habari ile, niliwashauri pia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), baada ya kuwa wamefanikiwa kupunguza ujinga wa waigizaji wa filamu wavaa nusu utupu, kuanza kukagua pia video za wasanii wa muziki wa kizazi kipya, kwani wapo wengine wanaojaribu kujitoa ufahamu, wakivaa Kimarekani wakati tunajua wazi kwao ni Kilosa.
Ni jambo linalotia faraja kuja kusikia kuwa BASATA, limeipiga marufuku video ya Snura ya wimbo wake mwingine, Nimevurugwa. Sijawahi kuiona video hiyo, lakini kwa namna ninavyomfahamu msanii huyu anavyoshughulika akiwa jukwaani, ni rahisi kuelewa kilichomo unaposikia kuhusu kuzuiliwa kwake.
Nichukue nafasi hii kuipongeza sana Basata, lakini wakati huohuo kutoa wito kwa chombo hicho cha serikali, kuangalia kwa jicho kali zaidi nyimbo nyingine zinazopigwa katika vituo vyetu vya televisheni, kwani wameruhusu ‘uzungu’ usio na maana kwa jamii, kana kwamba watu wanafuata maungo ya wacheza shoo badala ya kusikiliza ujumbe.
Inasikitisha kuona kwamba licha ya uchezaji huo wa kujidhalilisha, bado kuna msanii mwingine naye amemuiga karibu kwa kila kitu. Naye amekuwa akicheza na kuvaa kwa namna inayowadhalilisha sana mama zetu, lakini kwa namna ya kushangaza, wenyewe wamekuwa wakijisikia fahari na kuamini wanavutia.
Nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba wasanii wetu, hasa wale wanaobahatika kuwa nyota kwa kazi zao, wanapaswa kuwa mfano mbele ya jamii. Wanatakiwa wajue kuwa miongoni mwa mashabiki wa kazi zao, ni watoto wadogo, dada, kaka, shangazi na wazazi wanaojiheshimu. Unajaribu kujiuliza, hivi Snura anaweza kukata mauno kwa jinsi ile mbele ya wazazi wake?
Kwa vyovyote jibu la swali hili litakuwa ni hapana, vinginevyo labda awe na matatizo yasiyo ya kawaida kwenye kichwa chake. Sasa kama hawezi kucheza namna ile mbele ya wazazi wake, anajisikiaje anapofanya vile mbele ya wazazi wa wenzake?
Ni kweli biashara ni ubunifu, lakini inapendeza zaidi ubunifu wetu ukazingatia pia maadili yetu kama jamii yenye kuheshimiana. Uchezaji wa Snura jukwaani, unatoa ushawishi mkubwa kwa shabiki anayemsogelea kumshika makalio.
Mimi bado ni shabiki mkubwa wa maadili na ninaamini kutoka moyoni kwamba mashabiki wa muziki wa kizazi kipya wanavutiwa zaidi ya tungo kuliko uvaaji wa nusu uchi jukwaani.
Snura, Shilole na wasanii wengine wanaovaa na kucheza kihasara hasara, wanapaswa kubadilika kwa faida ya watoto wetu ambao utandawazi unaonekana kuwapoteza zaidi badala ya kuwasaidia!
GPL.