MWIGIZAJI wa Marekani, Eric Lawson maarufu kwa jina la Marlboro baada ya kutokea katika matangazo ya sigara miaka ya 1970 amefariki kwa ugonjwa wa mapafu akiwa na umri wa miaka 72.
Lawson alifariki Januari 10 mwaka huu akiwa nyumbani kwake San Luis Obispo kwa ugonjwa wa mapafu, kwa mujibu wa mkewe Susan Lawson.
Lawson aliyeanza kuvuta sigara akiwa na umri wa miaka 14, alionekana katika vipindi kadhaa vya TV vikiwemo, Baretta na The Streets of San Francisco ambapo baadaye alikodiwa kutangaza matangazo ya Marlboro kuanzia mwaka 1978 mpaka 1981 yaliyompatia umaarufu mkubwa.
Wakati wa uhai wake, Eric alicheza katika vipindi vilivyojizolea sifa vya Charlie's Angels, Dynasty na Baywatch.