Kigoma/Mbeya. Wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mikoa ya Kigoma na Mbeya wametoa misimamo tofauti juu ya kuvuliwa uongozi kwa Zitto Kabwe.
Wakati wafuasi wa Tawi la Mwandiga, Kigoma wakifanya maandamano kupinga kitendo hicho, wenzao wa Mbeya wameunga mkono hatua hiyo.
Kigoma
Baadhi ya wanachama wa Mwandiga walichoma moto kadi, bendera na fulana za chama hicho kupinga uamuzi wa kuvuliwa uongozi kwa Zitto.
Wanadaiwa kufanya vurugu hizo baada ya maandamano ya umbali wa kilomita tisa kutoka Mwandiga hadi Kigoma. Pia wanadaiwa kubomoa ukuta unaotumika kubandika matangazo.
Wakizungumza katika eneo la Kituo cha Mabasi Mwandiga, wanachama hao walisema Chadema kimekuwa na desturi ya kufukuza viongozi wanaopigania haki na kupambana na ufisadi nchini hatua ambayo walisema ni sawa na kudhoofisha jitihada za kupambana na uovu nchini.
Akisoma tamko lao, mmoja wa wanachama wa tawi hilo, Rucha Bakari alisema wanachama wa Kigoma wamepokea kwa masikitiko uamuzi wa chama kumvua madaraka Zitto na kusema jambo hilo linaua harakati za Chadema kuingia Ikulu mwaka 2015.
“Chama kimemdhalilisha kiongozi wetu Zitto Kabwe. Viongozi wa Chadema wamezidi kuonyesha ubabe na umangimeza dhidi ya viongozi wanaopigania haki za kidemokrasia ndani ya chama na rasilimali za chama,” inasema sehemu mojawapo ya tamko hilo na kuongeza:
“Walianza kwa kumfukuza Dk Aman Kabourou, David Kafulila, Shaibu Akwilombe, Habibu Mchange, Juliana Shonza na Mtella Mwampamba na sasa wamehamishia ukatili huo kwa mwanademokrasia, Jemedari wa vita dhidi ya ufisadi, Zitto. Ili chama kiwe na amani tunataka ufanyike mwafaka wa kitaifa ndani ya chama, vinginevyo tutachukua uamuzi mgumu.”
Mmoja wa viongozi wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Jimbo la Kigoma Kaskazini, Stumai Omari alisema anapinga uamuzi wa chama dhidi ya adhabu aliyopewa Zitto. Hata hivyo, alisema bado ataendelea kuwa mwanachama wa Chadema.
Tawi la Mwandiga ndiko alipozaliwa Zitto na kisiasa ndipo ilipo ngome kuu ya Chadema katika Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Mbeya
Uongozi wa Chadema kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kimetoa tamko la kuunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kumvua Zitto nyadhifa zote.
Mwenyekiti wa hamasa wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, David Mwangija ‘Mzee wa Upako’ alisema alipata taarifa za kuwapo kwa kundi moja la Chadema mkoani Mbeya ambalo lilikuwa likijiandaa kupinga kufukuzwa kwa Zitto na mwenzake na kwamba lilikuwa na mkakati wa siri ambao haukufahamika malengo yake.
Akifafanua kuhusu msimamo alioutaja kuwa ni wa Chadema mkoani Mbeya, alisema Zitto licha ya kuwa na nyadhifa za juu ndani ya chama ikiwamo Naibu Katibu Mkuu, alikuwa hashiriki kwenye shughuli nyingi za chama, jambo ambalo lilisababisha wamwone mzigo.
“Kwa niaba ya wanachama, wapenzi na mashabiki wa Chadema kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, sisi viongozi tunatoa tamko la kuunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu ya Chama chetu wa kumvua madaraka Zitto kwani tunaona hatua hiyo ilikuwa ni ya muhimu na pengine tunaweza kusema viongozi wetu walichelewa sana kuchukua hatua hiyo,” alisema Mwambigija.
Alisema Zitto alikwepa kushiriki mikutano ya Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (Movement for Change-M4C) iliyofanywa na chama hicho katika mikoa ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kusini, mikutano ya hadhara ya Chadema katika Mikoa ya Arusha na Dar es Salaam pamoja na kampeni ya kupinga Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba zilizofanywa na wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni.