-->
MALI zilizoachwa na aliyekuwa staa wa vichekesho Bongo, marehemu Hussein Ramadhani Mkieti ‘Sharo Milionea’ zinadaiwa kudhulumiwa na rafiki yake wa karibu aliyejulikana kwa jina moja la Suma, Risasi Jumamosi lina mkanda wote.
MADAI
Chanzo chetu kilichoongea na gazeti hili Julai 25, mwaka huu kilisema Suma anadaiwa kudhulumu mali za Sharo kufuatia kupewa madaraka ya kufuatilia na kuuza baadhi ya vitu bila fedha kumfikia mama wa marehemu, Zainabu Mkieti.
MAMA WA SHARO AFUNGUKA
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu Alhamisi iliyopita, mama huyo alikiri kuonekana kwa njama za Suma kudhulumu mali hizo likiwemo gari aina ya Opa lenye namba za usajili T 879 CAR na shilingi milioni 1. 2 za seti ya sofa alizonunua marehemu siku chache kabla ya kifo.
AZUNGUMZIA GARI
“Kweli nahitaji msaada ili nifanikishe kupata mali za mwanangu kwani kuna mambo hayaeleweki, kikubwa ni gari ambalo baada ya arobaini tulimpa Suma akaliuze kwa shilingi milioni kumi na moja na anipe fedha hizo lakini hadi sasa sijaona hata shilingi mia. Arobaini ya Sharo ilikuwa Januari 2013.
FEDHA ZA MASOFA
“Ukiachilia mbali gari, kuna fedha za masofa shilingi milioni moja na laki mbili sijazipata hadi leo, Suma aliahidi kunipa baada ya kuuza masofa hayo kwa dada yake na nimeshajaribu kuzungumza naye lakini hakuna majibu ya ukweli.
“Kabla ya Tuzo za Kili Music, Juni, mwaka huu, mimi nilikuja Dar na nikaongea na Suma na mama yake kuhusu fedha hizo, nilipomuuliza kuhusu gari, Suma akasema hataliuza na badala yake baada ya siku mbili angenitumia fedha lakini hadi leo hii simpati kwenye simu.
FEDHA ZILIKUWA ZITUMIKE KWA UJENZI
“Nakosa njia rahisi ya kuzipata fedha hizo maana huyu Suma naona kama mjanja, nilikuwa nataka kuanza ujenzi wa nyumba kwenye kiwanja alichokiacha marehemu lakini naona kama muda unakwenda,” alisema mama mzazi wa Sharo.
MAJIBU YA SUMA
Suma baada ya kupatikana kwenye simu yake ya kiganjani na kusomewa mashitaka hayo, alidai ameshaongea na mama Sharo lakini alisafiri na ni kweli alikuwa hapatikani kwenye simu.
“Mbona nimeshaongea na mama na mambo tumeyaweka safi, ujue nilikuwa South Africa (Afrika Kusini) nina kama wiki tatu tangu nirudi na kusema kweli sijawasiliana na mama Sharo ila tutamalizana tu mambo yakiwa vizuri,” alisema Suma.
KUMBUKUMBU
Sharo Milionea alifariki dunia kwa ajali ya barabarani Novemba 19, 2012 iliyotokea kwenye Kijiji cha Songa Maguzoni, Muheza Tanga akiwa ndani ya gari aina ya Harrier lenye namba za usajili T 378 BVR likitokea Dar es Salaam kwenda Tanga.
Alizikwa Novemba 23 kijijini kwao, Lusanga, Muheza, Tanga.
Source: GPL