MSANII wa Kundi la Kaole Sanaa, Zaina Ramadhan ‘Nandi’ anasumbuliwa na ugonjwa wa mifupa akidai kuvunjika pingili za mgongo kisha kushindwa kutembea na kufanya kazi zake za sanaa na nyinginezo.
Akipiga stori na mwandishi wetu hivi karibuni, Nandi alisema kuwa alianza kuumwa baada ya kupata hitilafu mwaka 2012 alipokuwa akitoka Chuo cha Sanaa pale Lego, Ubungo jijini Dar.
Nandi alisema siku ya tukio alikuwa akivuka barabara ambapo alishangaa kuona mguu umesita ghafla akashindwa kutembea hadi watu wakambeba kumsaidia kuvuka.
“Sikujua kilichonipata, nikaenda nyumbani wakanichua na mafuta ya asili ambayo yalinisaidia kidogo lakini tatizo lilizidi kuwa kubwa. Nikiwa nyumbani mama aliniomba nimsaidie kubeba vyombo lakini nilishindwa kuinua beseni baada ya kuinama na pingili za mgongo zikavunjika,” alisema Nandi.
Baada ya hapo, Nandi alisema alikwenda Hospitali ya Mwananyamala, Kinondoni jijini Dar ambapo alimuona daktari akamuandikia dawa za kutuliza maumivu na kumhamishia Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
“Hapa nilipo sina uwezo kabisa kwani dawa nilizoandikiwa zinauzwa ghali sana, familia imejitahidi kunisaidia lakini bado, nawaomba Watanzania wanisaidie ili nipate matibabu kwani sielewi tatizo langu ni nini kutokana na kukosa vipimo,” alisema Nandi.
Nandi amewahi kucheza filamu mbalimbali ikiwemo Yatima, Jua la Kiama, Kuzaa si Kupata na nyingine nyingi.
Kwa aliyeguswa na tatizo la msanii huyo na mwenye nia ya kumsaidia, awasiliane naye kwa namba 0684501177.